Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imesema kuwa bado
inaendelea kupokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali wa usafiri wa treni
inayofanya safari zake kati ya Stesheni na Pugu jijini Dar es Salaam.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja Mawasiliano wa
SUMATRA, Bw. David Mziray ambaye alibainisha kuwa kwa sasa bado wanaendela
kupokea maoni kutoka kwa wadau kama sheria ya mamlaka hiyo inavyoelekeza kabla
ya kuja na kiwango rasmi cha nauli ya usafiri huo.
“Tumetoa muda mpaka Agosti 19 mwaka huu iwe ndio
mwisho wa kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusiana na bei elekezi
ya nauli kwa treni inayofanya safari zake kati ya Stesheni na Pugu” Alisema
Mziray.
Pia, Mziray alifafanua kuwa kwa kipindi hiki ambacho
wanapokea maoni wameielekeza Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) waendelee kutoza
nauli ya shilingi 400 kwa watu wazima na shilingi 200 kwa watoto na wanafunzi
mpaka hapo itakapoamuliwa vinginevyo.
Alieleza kuwa tangu usafiri huo wa treni uanze
huduma zake imeonekana kuwapunguzia wananchi adha ya kusafiri muda mrefu njiani
na sasa wanaweza kuwahi katika maeneo yao ya kazi na biashara wakiwemo
wanaokwenda kwenye soko la Kimataifa la samaki la Ferry.
Aidha, aliongeza kuwa ili kuhakikisha wananchi
wanapata huduma hiyo ya usafiri pasipo na matatizo yoyote kampuni ya Reli
Tanzania (TRL) inatarajia kuongeza mabehewa kutoka 15 yaliyopo sasa hadi
kufikia mabehewa 20.
Akizungumzia baadhi ya changamoto walizoziona tangu
kuanzishwa kwa huduma hiyo ya usafiri wa Treni alisema kuwa ni pamoja na
ukosefu wa huduma ya vyoo na maji katika baadhi ya vituo.
“Tunatarajia hivi karibuni Kampuni ya Reli Tanzania
(TRL) itajenga vituo vipya na kufanya ukarabati kwenye vituo vya zamani ili kuweza
kuwaondolea usumbufu wananchi kwa kuweka huduma mbalimbali ikiwemo vyoo na maji
kwenye vituo hivyo” Alisema Mziray.
Treni ya Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) inayofanya
safari zake kati ya Stesheni na Pugu ilizinduliwa hivi karibuni na Waziri wa
Ujenzi ,Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa na imekuwa msaada mkubwa
kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam hasa wakazi wa maeneo ya Gongolamboto, Pugu na Chanika.
MWISHO.
Na Abushehe Nondo (MAELEZO).
No comments:
Post a Comment