RAIS John Magufuli amevunja Kamisheni ya Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) na kuwasimamisha kazi watendaji wakuu wa tume hiyo baada ya kubainika kudahili wanafunzi wasio na sifa na kuwapa mikopo.
Pia serikali imetangaza kufanyika kwa udahili upya Vyuo
Vikuu vyote nchi nzima ili kuwaondoa vyuoni wanafunzi wote wasio na sifa
sambamba na kutangaza vita kali kwa wanafunzi hewa wanaopata mikopo ya elimu ya
juu.
Hayo yamebainishwa leo na Prof. Joyce Ndalichako Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia alipozungumza na waandishi wa habali juu ya
kuvunjwa kwa Kamishina ya TCU.
Amesema, kwa idhini aliyopewa na rais anawasimamisha
kazi mara moja watendaji hao wa Kamisheni ya Tume ya Vyuo
Vikuu.
Prof. Ndalichako amewataja waliosimamishwa kazi kuwa ni
Prof. Yunus Mgaya, Katibu Mtendaji wa TCU kwa kushindwa kusimamia kazi za TCU
akiwa kama mtendaji mkuu wa taasisi hiyo.
Pia, Dk. Savius Maronga, Mkurugenzi wa Udhibiti na
Ubora kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake wa kusimamia ubora na ithibati ya
Vyuo Vikuu.
Amesema Rose Kiishweko, Mkurugenzi wa Udahili
amesimamishwa kwa kushindwa kusimamia udahili wa wanafunzi na kupelekea
kudahiliwa wanafunzi wasio na sifa, na mwingine aliyesimamishwa ni Kimboka
Istambuli ambaye alikuwa Kaimu Mkurugenzi wa Udahili na
Nyaraka.
Mbali na hilo Prof. Ndalichako amesema, ili shughuli za
TCU ziendelee, Prof. Eliuter Mwageni ameteuliwa kukaimu nafasi ya katibu
mtendaji na kabla ya uteuzi wa kukaimu nahfasi hiyo Prof. Mwageni alikuwa Naibu
Makamu Mkuu (Utawala na Fedha) wa Chuo Kikuu cha Ardhi.
Aidha ameteuliwa Dk. Kokubelwa Mollel ambaye atakaimu
nafasi ya ukurugenzi wa udahili na nyaraka na kabla ya uteuzi wa kukaimu nafasi
hiyo Dk. Kokubelwa alikuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Amesema kwa muda mrefu kumekuwa na taarifa za wanafunzi
wa Chuo Kikuu cha St. Joseph wanaodahiliwa kutokuwa na sifa.
Waziri amesema, kutokana na hilo serikali imeamua kutoa
tamko baada ya ukaguzi kufanyika katika chuo hicho katika kampasi za Arusha na
Songea na kubaini kuwepo kwa upungufu mkubwa katika utoaji wa elimu isiyokuwa na
kiwango.
Amesema, walibaini kuwepo kwa wanafunzi 489 ambao wapo
katika vyuo hivyo ambao hawakidhi viwango na hawana sifa za kusoma Chuo
Kikuu.
Amesema kibaya zaidi ni kuwepo kwa wanafunzi ambao ni
wa kidato cha nne waliofaulu Daraja la Nne huku wengine wakiwa na pointi 32
lakini wakidahiliwa kusomea shahada ya kwanza .
“Mwanafunzi wa Kidato cha Nne anasoma digrii ya
Sayansi, huku mtu huyo akiwa sekondari kasoma mkondo wa biashara lakini
kadahiliwa asomee Sayansi na analipiwa mkopo na TCU.
“Si tu hana sifa ya kusoma Chuo Kikuu, hana hata
sifa ya kuwa na cheti cha ualimu kwa maana hiyo mtu wa aina hiyo hafai hata
kuwa na cheti cha ualimu hatuwezi kukubali mtu wa jinsi hiyo akasomee digrii,”
amesema.
Prof. Ndalichako amesema rais amekuwa akihangaika
kutafuta fedha kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu lakini cha kusikitisha kuna
wanafunzi waliofaulu vizuri Kidato cha Sita wanakosa mikopo ila wale waliofeli
wanapata mikopo hiyo.
“Divisheni four pointi 34 yuko Chuo Kikuu hata
ualimu simkubali mtu wa namna hiyo,” amesema.
Amesema, baada ya serikali kufunga chuo hicho wanafunzi
hao walihamishiwa vyuo vingine lakini hata huko walikopelekwa uwezo wao
umeonekana kuwa ni mdogo hali iliyolazimu kuwarudisha madarasa ya
nyuma.
‘Wanafunzi waliotoka St. Joseph na kupelekwa Chuo
Kikuu cha Dodoma uwezo wao umeonekana kuwa ni mdogo, ambapo wanafunzi wa mwaka
wa pili na wa kwanza wamerudishwa nyuma muhula moja huku wale wa mwaka wa tatu
wamerudishwa nyuma mwaka moja” amesema.
Amesema, wale wa St. Joseph Tawi la Songea
waliopelekwa Chuo Kikuu cha Kilimo Morogoro (SUA) waliokuwa wakisoma mwaka wa
nne wamerudishwa mwaka wa tatu na wametengewa vipindi vya ziada ili kurekebisha
upungufu huo, na hata wale waliopelekwa vyuo vingine vya Ruaha, Mkwawa
wameonekana kuwa na upungufu pia.
“Kibaya zaidi hao wanafunzi walikuwa wanapata
mikopo, Division four anapata mkopo haki iko wapi, tulipoona jambo hili si sawa,
tulichukua hatua tukaieleza bodi ya TCU kusimamisha kazi waliohusika lakini hilo
halikufanyika,” amesema.
Kufuatia kuwepo kwa matatizo hayo Prof. Ndalichako
ametangaza vita kwa vyuo mbalimbali ambavyo vina watu ambao wanadahili wanafunzi
wasio na sifa.
Kuhusu wanafunzi ambao hawakuwa na sifa lakini walikuwa
wakisoma chuo kikuu hicho amesema licha ya kuwa wamepoteza muda wao mwingi
lakini watalazimika kurejesha mikopo hiyo.
“Wale wote ambao walipata mikopo bila kuwa na sifa
watarejesha mikopo hiyo na hakuna njia yoyote ya kuwasaidia bali wanatakiwa
kuendelea kuangalia ni jinsi gani ya kujiendeleza,” amesema.

No comments:
Post a Comment