Muungano wa upinzani nchini Kenya umeahirisha
kwa muda maandamano ambayo umekuwa ukiandaa kila wiki katika miji mikuu nchini
humo.
Mmoja wa viongozi wa muungano huo, Seneta wa Machakos Johnstone Muthama, amesema uamuzi wa kuahirisha maandamano hayo umechukuliwa kuipa serikali muda wa
kuitisha mazungumzo.
Muungano huo wa Coalition for Reforms and Democracy (CORD), umeipa
serikali makataa ya siku 10 la sivyo urejelee maandamano hayo.
Viongozi wa CORD wanataka maafisa wakuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC)
wajiuzulu, wakisema tume hiyo haiwezi kuandaa uchaguzi mkuu huru na wa haki mwaka
ujao. Jumatatu wiki hii, mmoja wa waandamanaji alifariki kwenye maandamano mjini
Kisumu, magharibi mwa Kenya. Msemaji wa serikali Eric Kiraithe Jumanne aliwaambia wanahabari kwamba, maafisa
29 wa polisi walijeruhiwa wakati wa maandamano hayo. Serikali hiyo imesema maandamano hayo ni haramu.
No comments:
Post a Comment